Joto la mwili wako linapokuwa juu ya kiwango cha kawaida cha 37.5 ° C, utakuwa una homa. Ukiwa katika hali hii, mwili wako unahisi joto kuliko kawaida na wakati mwingine hutetemeka au huhisi baridi.
Mara nyingi, homa ni dalili ya ugonjwa na si ugonjwa wenyewe. Hii ndiyo sababu humfanya daktari kutambua sababu ya homa. Homa pia ni mwitikio wa asili wa mwili kwa magonjwa yanayoathiri mwili. Unapokuwa na homa inamaanisha kuwa mwili wako unajaribu kupambana na virusi au bakteria ambao wanaweza kuwa wamesababisha maambukizi.
Unaweza kutambua iwapo una homa kwa kutumia kipima joto, ambacho kawaida huwekwa kwenye kwapa au kinywani chini ya ulimi wako kwa dakika tatu. Kwa watoto, kinaweza pia kuwekwa kwenye kwapa au sehemu ya haja kubwa.
Kutokana na kukua kwa teknolojia watu wengi hutumia kipima joto cha dijiti.
Visababishi vya homa
Sababu za homa zinaweza kutoka ndani au nje ya mwili. Vijidudu vinavyosababisha magonjwa kama bakteria vikiingia mwilini mwako, vinaweza kutoa kemikali zenye sumu. Hali hii inaweza kuufanya mwili ujiweke tayari kukabiliana na hali ya magonjwa yanayoiathiri mwili. Hapa ndipo homa huanzia, kwa mfano ukiwa na:
- Malaria –hii husababishwa na vimelea kupitia kuumwa na mbu
- Dengue – inasababishwa na virusi kupitia kuumwa na mbu
- Homa ya mafua – inayosababishwa na virusi na kawaida huambukizwa hewani, homa ya mapafu au COVID-19
- Kuvimba kwa tonsil- hii husababishwa na bakteria au virusi
- Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)
- Sababu nyingine – kukua kwa meno, kwa watoto n.k
Ni wakati gani umuone daktari?
- joto la mwili likiwa ni zaidi ya 38 ° C.
- ukiwa na dalili za malaria kama vile maumivu ya kichwa, kutapika na kuharisha pamoja na maumivu ya viungo
- ukiwa na kinywa kikavu na umepunguza mzunguko na kiwango cha mkojo
- unapokuwa mwepesi na dhaifu
- unapokuwa kwenye matibabu kwa sababu ya kinga ndogo (upungufu wa kinga)
- unatumia dawa kama vile steroids zinazoshusha kinga ya mwili
- uko kwenye matibabu ya hivi karibuni ya saratani
- umefanyiwa upasuaji wa kupandikiza hivi karibuni
- una ugonjwa sugu wa mapafu
- una pumu, ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa kisukari, ugonjwa sugu wa ini, au ugonjwa wa seli mundu
Matibabu ya homa
Mara nyingi, homa hutoweka baada ya siku chache haswa pale inapokuwa zimesababishwa na virusi. Unaweza kufanya yafuatayo kupunguza homa:
- Epuka kuvaa nguo nyingi kwa wakati mmoja kupita kiasi
- Hakikisha uko katika chumba chenye hewa ya kutosha kisicho na joto sana
- Kunywa maji mengi
- Epuka kunywa pombe
- Waweza kutumia dawa yakupunguza homa, kama paracetamol
Kumbuka: Homa kwa watoto (chini ya miaka mitano) inapaswa kuchukuliwa kwa dharura sana. Homa isipothibitika haraka inaweza kusababisha madhara makubwa. Katika hali kama hiyo, matibabu ya haraka yanahitajika.
Jinsi ya kuzuia homa
Kwa kuwa homa hutokea pale mwili unapovamiwa na vimelea vinavyoweza kusababisha maambukizi, unaweza kufanya yafuatayo ili kukusaidia kuzuia:
- Nawa mikono yako mara kwa mara kwa kutumia maji safi na sabuni
- Unaweza kubeba dawa ya kusafisha mikono ili mikono yako isiwe na vijidudu
- Daima tumia kitambaa kufunika mdomo wako wakati unakohoa na pua yako unapopiga chafya
- Epuka kushiriki vyombo vya kula na watu wengine