DEGEDEGE KWA WATOTO

  • DEGEDEGE NI NINI?

Degedege ni hali isiyokuwa ya hiari, inayohusisha kutetemeka, kutikisika na kukamaa kwa viungo vya mwili inayosababishwa na hitilafu kwenye ubongo. Inaweza kuambatana na kuzungusha macho kuelekea juu, kutoa povu mdomoni, kung’ata ulimi na midomo, kupoteza fahamu, kushindwa kuzuia haja ndogo au/na kubwa na kupoteza kumbukumbu kwa muda. Degedege inaweza kumpata mtu wa umri wowote lakini watoto ni kati ya makundi yaliyopo hatarini zaidi kupata degedege.

  • DEGEDEGE KWA WATOTO HUSABABISHWA NA NINI?

Zifuatazo ni baadhi ya sababu za degedege kwa watoto;

  • Homa au maambukizi ; mfano malaria, homa ya uti wa mgongo n.k
  • Kifafa
  • Kuumia kichwani
  • Kemikali za mwili zisipokuwa kwenye uwiano sahihi mfano; kiwango cha sukari kwenye damu kushuka chini ya kawaida (hypoglycemia)
  • Sumu
  • Uvimbe kwenye ubongo
  • Kiharusi
  • Baadhi ya dawa
  • Pombe au dawa za kulevya
  • NINI CHA KUFANYA AU KUTOFANYA ANDAPO MTOTO WAKO ATAPATA DEGEDEGE?

Cha kufanya

  • Mfungue nguo au vitu vya kubana hasa maeneo ya shingoni na kichwani ili kumuwezesha kupumua vizuri na kuepuka kukabwa
  • Hakikisha yupo kwenye mazingira salama
  • Endapo atatapika mlaze upande na umsafishe
  • Mpeleke mtoto hospitali haraka kwa uchunguzi zaidi

           Usifanye haya:

  •  Kumshikilia kwa nguvu  mtoto akiwa katika hali ya degedege
  • Usimuwekee kitu chochote mdomoni
  • Usimuache mtoto peke yake akiwa na degedege au mara baada ya degedege kuisha
  • MATIBABU YA DEGEDEGE NI YAPI?
  • Endapo mtoto wako ataonyesha dalili za degedege muwahishe hospitali kwaajili ya uchunguzi zaidi hata kama ile hali itakuwa imeiisha.
  • Huduma ya kwanza atakayopewa mtoto itategemea na hali yake kwa wakati ule, ikiwa bado atakuwa na hali ya degedege atapewa dawa za kuituliza.
  • Maelezo ya mzazi jinsi degedege ilivotokea na hali ya mtoto yatamuongoza mhudumu wa afya kupanga vipimo vya kufanya.
  • Baadhi ya vipimo anavyoweza kufanyiwa ni pamoja na kiasi cha sukari kwenye damu, malaria, kuangalia dalili za maambukizi kwenye damu (full blood picture), kupimwa maji ya uti wa mgongo, kipimo cha umeme wa kichwa (EEG), CT scan ya kichwa, MRI n.k
  • Kumbuka kuwa mhudumu wa afya anategemea sana maelekezo yako ili kujua vipimo vya kumfanyia mtoto na kupangiia tiba ili kuokoa maisha ya mtoto. Hivyo ni vyema kueleza kwa ufasaha historia ya ugonjwa hata kama unahisi kuna uzembe ulijitokeza; mfano mtoto alikosa uangalizi akadondoka na kuumia kichwani au pombe / dawa /sumu ziliachwa sehemu ambayo mtoto aliweza kufikia akanywa.
  • MADHARA YA DEGEDEGE KWA MTOTO
  • Kuumia endapo itamtokea akiwa kwenye mazingira hatarishi kama akiwa karibu na moto au akiwa kwenye maji
  • Madhara ya kudumu kwenye ubongo wa mtoto endapo itatokea mara kwa mara na ikakaa kwa muda mrefu
  • JINSI YA KUMKINGA MTOTO WAKO DHIDI YA DEGEDEGE
  • Endapo mtoto ana kifafa au anatumia awa za kuzuia degedege hakikisha anakunywa dozi aliyoandikiwa na daktari na kwa wakati.
  • Mtoto akiwa na homa apewe dawa za kushusha homa na mpeleke hospitali kwa uchunguzi na matibabu zaidi
  • Mtoto akiwa mgonjwa na yupo kwenye matibabu lakini hawezi kula, anatapika kila kitu mrudishe hospitali kwa msaada zaidi.
  • Epuka kuweka dawa, pombe au sumu maeneo ambayo yanaweza kufikiwa na mtoto.
  • Mazingira ya kucheza mtoto yawe salama
MedicoPRESS
MedicoPRESShttp://www.researchcom.africa
MEDICOPRESS is a Non-Governmental Organization that promotes Medical Journalism, Professional Development and Public Health Education. It’s a network of medical scientists and journalists who believe in the dissemination of accurate medical/ health inform information in the process of imparting positive changes in the community.

Subscribe

Related News

- Advertisement -spot_img

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here